30 Septemba 2025 - 11:48
Source: ABNA
Umoja wa Ulaya Warudisha Tena Vikwazo Dhidi ya Iran

Siku moja baada ya kuanzishwa tena kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya ulirudisha tena seti ya vikwazo dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahl-ul-Bayt (a.s.) - Abna, Umoja wa Ulaya leo Jumatatu ulitangaza kurudisha tena seti ya vikwazo dhidi ya Iran vinavyohusiana na shughuli zake za nyuklia. Uamuzi huu ulikuja siku moja baada ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Tehran kurejeshwa kiotomatiki.

Vikwazo vya Ulaya ni pamoja na kupiga marufuku usafirishaji wa silaha, vifaa vinavyohusiana na urutubishaji wa uranium, na makombora ya balistiki. Pia, vizuizi kama vile marufuku ya kusafiri, kufungia mali za watu na taasisi za Iran, na vikwazo vya kifedha na biashara dhidi ya mafuta, gesi, na bidhaa za petroli za Iran vimerudishwa.

Katika mfumo huo huo, mali za Benki Kuu ya Iran na benki zingine kubwa za Iran katika Umoja wa Ulaya zilifungwa tena, na safari za ndege za mizigo za Iran zilipigwa marufuku kuingia kwenye viwanja vya ndege vya EU.

Hatua hii ilichukuliwa baada ya Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani (Troika ya Ulaya) kutumia Utaratibu wa Kurejesha Vikwazo (Snapback Mechanism) katika makubaliano ya nyuklia ya 2015; utaratibu unaoruhusu kurejeshwa kiotomatiki kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa. Juhudi za pamoja za Urusi na China kuzuia mchakato huu katika Baraza la Usalama ziligonga mwamba.

Taarifa ya Nchi Tatu

Ufaransa, Ujerumani, na Uingereza zilitangaza katika taarifa ya pamoja kwamba lengo lao kuu ni kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia. Nchi hizi ziliishutumu Iran kwa kukiuka ahadi zake mara kwa mara na zikasema kwamba hazikuwa na budi ila kuamsha Utaratibu wa Kurejesha Vikwazo.

Hata hivyo, zisisitiza kwamba bado zimejitolea kwa diplomasia na zinataka kuanza tena kwa mazungumzo. Taarifa hiyo pia iliitaka Iran kujiepusha na hatua zinazosababisha kuongezeka kwa mvutano na kuzingatia majukumu yake ya kimataifa.

Mwitikio wa Iran

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Abbas Araghchi, aliuita uamuzi huo kuwa haramu na, katika barua kwa wenzake katika nchi kadhaa duniani, alitaka hatua kama hizo zikataliwe. Huku akisisitiza utayari wa Tehran kwa mazungumzo, alitangaza kwamba Iran itasimama imara dhidi ya ukiukwaji wowote wa haki na maslahi yake halali.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, pia alikemea kurejeshwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa na kusema kwamba Tehran iko tayari kukabiliana na hali yoyote na haitaingia katika mazungumzo yanayosababisha migogoro mipya.

Your Comment

You are replying to: .
captcha